In Summary
  • Nnauye alifiti katika wizara hiyo kwa kile alichokuwa akikifanyia kazi kwa kuwa alikuwa ni mtu wa michezo. Enzi zake waziri huyo alifanya kazi nyingi bila ya upendeleo wa timu wala kuegemea katika michezo mingine mbali na soka.

NAFAHAMU Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli alimteua Nape Nnauye kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, katika baraza lake la kwanza la mawaziri.

Nnauye alifiti katika wizara hiyo kwa kile alichokuwa akikifanyia kazi kwa kuwa alikuwa ni mtu wa michezo. Enzi zake waziri huyo alifanya kazi nyingi bila ya upendeleo wa timu wala kuegemea katika michezo mingine mbali na soka.

Lakini baadaye Rais Magufuli alimteua, Harrison Mwakyembe kushika nafasi hiyo. Pamoja na Mwakyembe kuwa mwanasheria anafanya vizuri kwa kuwa Tanzania sasa inakwenda kuwa mwenyeji wa Afcon ya U-17.

Hata Mwakyembe naye amekuwa akishiriki katika michezo mingine mbali na soka kwa kuweza kuhakikisha mambo yanakwenda sawasawa.

Katika awamu yake ya kwanza, Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimteua, Hassan Wario kuwa waziri wa michezo.

Katika kuongoza kwake wizara hiyo, Wario, Kenya imepoteza nafasi ya kuandaa mashindano ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani (Chan).

Jambo hili halikuwapendeza Wakenya wengi. Walihuzunika kwa kukosa kuandaa mashindano hayo ambayo yangeweza kulitangaza taifa la Kenya na Afrika Mashariki kwa jumla.

Sio wananchi wa Kenya tu waliu,ia kwa taifa lao kushindwa kuandaa mashindano hayo, bali hata wale wa Uganda na Tanzania nao walijisikia vibaya sana.

Ndio wananchi wa nchi hizo jirani walijua wangeweza kuyashuhudia kwa ukaribu mashindano hayo ambayo mara nyingi hufanyika mbali na ukanda wetu, hivyo kushindwa kwenda kutokana na gharama kubwa.

Baada ya Wario kutuhangaisha Rais Kenyatta akafanya mabadiliko, akamleta Rashid Echesa. Bahati mbaya Echesa hakuwa akifahamu lolote katika shughli za michezo.

Zaidi ya mwaka mmoja ofisini hakuna lolote la maana alilolifanya. Ameingia kwenye siasa za kumtafutia kura Makamu wa Rais mwaka 2021.

Juzi wachezaji wa vikapu wameenda Rwanda kwa njia ya barabara katika Mashindano ya Bara la Afrika. Timu ilisafiri zaidi ya masaa 48 kwa barabara!

Kama haitoshi vifaa vya wanariadha vya kutumia katika mashindano ya Olimpiki vimepatikana kwenye nyumba ya baadhi ya wafanyikazi wa wizara ya michezo.

Wengine walikuwa wakiviuza. Wanamichezo Kenya hawana haki kabisa. Ni jambo la kukera sana. Na wakati niliposkia Echesa anaachishwa kazi, nikashukuru. Lakini wakati huohuo, nikasikitika tena wizara hiyo kupewa Amina Mohammed.

Nikijaribu kuangalia rekodi yake ya kimichezo sioni. Tumechezwa tena. Ombi langu kwa marais wa Afrika Mashariki wanapotaka kuwateua mawaziri wa michezo wawaite wahusika wote wa michezo awakalishe chini awaulize wizara hizo wanafikiria ni kina nani wanaweza kuziongoza vizuri.

Kuna michezo mingi tu katika kanda yetu ya Afrika Mashariki kama vile ndondi, soka, riadha, vikapu, mpira wa mikono, voliboli na mingine mingi tu kwa hiyo washiriki wanaweza kuwa wengi kiasi cha kutosha.

Marais wa Kenya, Tanzania na hata Uganda wanaweza kufanya mijadala na viongozi wa michezo hiyo na kuwauliza ni kina nani wanafaa kupewa wizara hiyo.

Kwa njia hiyo, naamini wanaweza kupatikana watu wanaoweza kuwatatetea wanamichezo bungeni na watakaowasaidia michezo kukua katika kanda yetu. Ikumbukwe kiongozi ambaye amewahi kushiriki michezo anafahamu uchungu wake na anaweza kuwasaidia inavyostahiki wanamichezo wote bila ya kuwabagua.

Hapo tunaweza kupata mawaziri wa michezo ambao wanajali maisha ya wanamichezo. Watu ambao tayari wameshawahi kushiriki michezo wanaweza kusikia uzito ambao wanamichezo wanapitia, ndio wanapaswa kuziongoza wazara hizo.

Kulala njaa, kuingia uwanjani bila lishe, kutembea hadi mazoezini kwa kukosa nauli, kukosa vifaa vya michezo vinavyovihitajika.

Watu kama hawa watafanya kazi kwa kujali ubinaafamu. Kwa kutuletea watu ambao hawafahamu lolote katika michezo kwa kweli inakera sana.

Rubani wa ndege abaki kuwa rubani, injinia abaki na kazi yake. Hauwezi kuwaleta watu ambao hawafahamu lolote kuhusu michezo kuwaongoza wanamichezo.

Kwa Tanzania mambo yanaenda poa sana chini ya Waziri Mwakyembe lakini kwa Kenya, naona waziri mpya wa michezo akikosa tena kutekeleza majukumu yake.

Kenya ilipoteza kuandaa mashindano ya Chan baada ya viongozi wa Caf kutoridhishwa na matayarisho yetu.

Viwanja ambavyo vilihitajika kutengeneza ili kuaandaa mashindano hayo havikutengenezwa.

Shida kubwa ni waziri wa michezo alila katika shughli hiyo. Kulihitajika kutengenezwa angalau viwanja vitano tu lakini hamna hata kimoja kilichotengenezwa.

Kenya imekuwa ikiona waariadha wengi tu wakihangaika. Juzi tu timu ya wanasoka walemavu walihangaika kupata hela tu za kuenda mashindano ya walemavu Brazil.

Tuache kupiga siasa katika michezo kwa kuwa ni mojawapo ya vitega uchumi mkubwa sana duniani.

Kama kweli Afrika Mashiriki tukiamua kuangazia fani hizi za michezo na kuwa na umoja, tunaweza kufika mbali sana kimataifa.

ADVERTISEMENT