UNAUKUMBUKA mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba na Yanga msimu uliopita? Ndio, ule uliopigwa Uwanja wa Uhuru na timu hizo watani wa jadi kutoka sare ya bao 1-1.

Simba ilipata bao lake lililofungwa na Shiza Kichuya, huku la Yanga likifungwa na Obrey Chirwa ambaye kwa sasa anakipiga Azam FC.

Mchezo ule ulikuwa ni moja ya michezo mizuri sana kwa watani hao na kama utaenda kuangalia tena mkanda kwa kilichofanyika siku hiyo, ni wazi utapata rundo la wachezaji waliocheza vizuri.

Kuanzia langoni, Aisha Manula wa Simba alionyesha kiwango bora, mabeki wa pembeni na wa kati, Erasto Nyoni wa Simba na Kelvin Yondani wa Yanga, walikuwa bora huku eneo la kiungo likitendewa haki na Jonas Mkude na Papy Kabamba Tshishimbi.

Kule mbele ndiko kulikuwa na shughuli na huku kuna baadhi ya waliofanya vyema.

Hata hivyo, turudi kwenye eneo la kiungo hasa kiungo cha chini au mkabaji. Kwenye mcheo huo siku hiyo kulikuwa na vita kubwa kati ya kiungo ya Simba ambao kwa kawaida hucheza wanne au watatu.

Siku hiyo kulikuwa na viungo watatu Haruna Niyonzima, James Kotei na Jonas Mkude huku upande wa Yanga ukiwa na Papy Tshishimbi na Rafael Daudi pamoja na Pius Buswita.

Jicho la watanzania wegi lilikuwa likimuangalia zaidi mchezaji mpya wa Yanga, Papy Tshishimbi ambaye siku hiyo alifanya kazi kubwa huku akionyesha ufundi mkubwa mbele ya viungo wa Simba.

Tshishimbi alikuwa kwenye kiwango kizuri akijitahidi kunyang’anya mipira na kupandisha mashambulizi.

Wengi walisema alikuwa akihaha tu uwanjani ingawa ni wazi kazi yake bora wenzake walishindwa kuitendea haki.

Kiwango chake kilikuwa kikubwa kuliko wenzake na hivyo kushindwa kutengeneza uwili au utatu wa viungo wa katikati na kusababisha wakati mwingine kutoona ule ubora wake tuliokuwa tukiutegemea.

Sio mchezo huo, Tshishimbi amecheza michezo mingine mingi tu vizuri na kushangaza watu kwa jinsi alivyo mwepesi kuzioea viwanja mbalimbali vya Tanzania hata vile ambavyo sio bora kwa kuchezea.

Alicheza vizuri Uwanja wa Sabasaba mjini Njombe, Uwanja wa Majimaji, Songea ambao siyo rafiki kabisa kuchezea na alivyokwenda Kambarage, Shinyanga, ndiye alikuwa injini ya Yanga na kweli aliibeba mabegani kwake.

Hata hivyo, kwa muda mrefu alicheza kama namba nane kiungo wa juu ingawa na kiuhalisia ni mzuri akicheza kama kiungo wa chini.

Siku zinakwenda kasi na sasa Tshishimbi anakumbwa na majeraha ya mara kwa mara, huku pia akikumbwa na tatizo la kifedha kama ilivyo kwa wenzake msimu huu.

Matatizo haya huenda yakawa yanaonekana wazi machoni kwetu ndiyo yanachangia kushuka kwa kiwango cha Tshishimbi ingawa kuna mengine huenda yamejificha nyuma ya pazia, hasa kutokana na sababu nyingi tunazoziona kwa mchezaji huyu.

Kuna tofauti kubwa kati ya Tshishimbi huyu na yule wa mwanzoni alivyotua tu Yanga.

Wa sasa anaonekana hana stamina ya kumfanya anyumbulike uwanjani. Anapoteza sana pasi na hayuko sawa kwenye umiliki wa mpira, huku pia kisaikolojia akiwa si salama. Kwa jumla anaanza kuondoka taratibu kwenye ushindani wa namba kwenye nafasi ya kiungo.

Ni wazi Tshishimbi alishakuwa kioo kwa wachezaji wetu wa Tanzania kama alivyowahi kuwa Haruna Niyonzima huko nyuma na sasa Cletous Chama.

Tshishimbi anatakiwa kujitathimini sana na kuamua kwa dhati kurudi kwenye ile thamani aliyoionyesha siku za mwanzo mwa msimu uliopita.

Inawezekana yapo mengi tusiyoyajua ama yanamfanya apotee ambayo si halali na mengine ya halali.

Hata hivyo, nionavyo Tshishimbi kwanza anatakiwa kurudi kwenye uwezo wake wa awali wa uchezaji kwa kufanya mazoezi sana, kupata muda mwingi wa kupumzika, pia kutunza mwili wake. Anatakiwa kujitathimini sana na kuamua kwa dhati kurudi kwenye ile thamani aliyoionyesha siku za mwanzo mwa msimu uliopita.

Aidha anatakiwa kukubali yeye ni mchezaji kiungo wa chini na siyo kiungo mshambuliaji au mchezeshaji na wakati mwingine akitaka kucheza juu kama mshambuliaji namba mbili atapotea kabisa uwanjani.

ADVERTISEMENT