In Summary
  • Aprili 6, Kamati ya Rufaa ya TFF ilitangaza rasmi kumfungia Wambura kutojihusisha na soka katika maisha yake yote kwa kosa la kuchukua na kupoka fedha za TFF za malipo ambayo yalidaiwa kutokuwa halali kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanuni za maadili za TFF Toleo la 2013.

SAKATA la aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura limefika tamati baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania kuamuru bosi huyo arejeshwe kwenye nafasi yake kwenye shirikisho hilo.

Aprili 6, Kamati ya Rufaa ya TFF ilitangaza rasmi kumfungia Wambura kutojihusisha na soka katika maisha yake yote kwa kosa la kuchukua na kupoka fedha za TFF za malipo ambayo yalidaiwa kutokuwa halali kinyume na kifungu cha 73(1) cha kanuni za maadili za TFF Toleo la 2013.

Ilielezwa vitendo hivyo vinaishusha hadhi TFF ikiwa ni kinyume na Ibara ya 50(1) ya Katiba ya TFF kama ilivyorekebishwa mwaka 2015, huku ikimruhusu Wambura kupeleka malalamiko yake kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kama hakuridhishwa na hukumu hiyo.

Kwa upande wa Wambura anadai hakuna sehemu inayomuongoza kwenye CAS bali Kamati ya Rufaa ya TFF ni sehemu ya mwisho kwa Wambura kujitetea.

Wambura alikwenda Mahakama Kuu ya Tanzania ambako alipeleka malalamiko yake ambayo yamesikilizwa na kutolewa uamuzi wa kutengua hukumu hiyo kwa madai hukumu yake haikuzingatia taratibu za kisheria, hivyo arudishwe kuendelea na majukumu yake.

Nafasi ya Wambura baada ya kufungiwa ilichukuliwa mshindani wake katika Uchaguzi Mkuu wa TFF, Athuman Nyamlani ambaye alikuwa akikaimu hadi hapo uchaguzi mdogo utakapofanyiwa huku tetesi zikisema kwenye nafasi hiyo Nyamlani angegombea pamoja na Almas Kasongo ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA).

Uchaguzi wa kujaza nafasi mbalimbali ndani ya shirikisho hilo umepangwa kufanyika Februari 2, mwakani.

Baada ya Mahakama Kuu kutengua adhabu ya Wambura ambaye pia alikuwa ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara, anapaswa kurudi kazini huku Nyamlani akitakiwa kukabidhi ofisi hiyo aliyokabidhiwa na Rais, Wallace Karia.

Kitu pekee ambacho pia kinaleta mkanganyiko kwa wadau wa soka nchini ni juu ya utendaji kazi kati ya Wambura na bosi wake Karia ambapo kwa haya yanayoendelea inaonyesha wazia hawaivi chungu kimoja, hivyo ni lazima mambo yanaweza kuharibika muda wowote.

Ingawa Mahakama Kuu imetoa uamuzi huo, badala ya CAS ambapo uamuzi wa mahakama hautenguliwi na mtu yeyote unawaweka njia panga wote wawili Wambura na TFF katika kupeana majukumu ingawaje Makamu wa Rais ndiye mshauri mkuu wa Rais sidhani kama kuna ushauri utakaotolewa kwake na ukafanyiwa kazi kama ilivyo sasa kati ya Karia na Nyamlani.

Hatujui nyuma ya pazia kuna nini, ila inaonyesha kuna jambo ambalo wawili hawa (Karia na Wambura) wanaonyesha kama kutaka kufanya kazi kwa kukomoana kwa mambo binafsi ama kama sio binafsi, basi kwa kutofuata sheria, kanuni na katiba yao.

Bado kuna maswali kwenye vichwa vya watu, Je, Wambura alifikaje kwenye ofisi za shirikisho hilo baada ya hukumu yake kutolewa na Mahakama Kuu?

Moja ya maswali yanayogonga vichwa ni wawili hao watafanyaje kazi kwa sababu wameonekana kutokuwa na mawasiliano mazuri? Itakuwaje Wambura atakapoanza kufanya majukumu yake, atawasiliana vipi na bosi wake ili majukumu yaende vizuri?

Lakini Wambura ameonekana kutokuwa na hofu, amekuwa akijiamini kupita maelezo na kudai anastahili kuwa hapo alipo ama kuwepo hapo ambapo mahakama imeamuru awepo.

Bado pia inagonga vichwani mwa watu wengi kuhusu hukumu hiyo kwanini isingepelekwa CAS na ikapelekwa mahakamani tena isiyo ya kimichezo, ila inadaiwa awali, Wambura alifanya taratibu zote za kwenda CAS lakini aligonga mwamba ndiyo maana aliamua kutafuta haki yake mahakamani.

Wambura ameweka wazi kuwa amepeleka nyaraka zake TFF na kupokelewa kwake kunaashiria kukubaliwa kwa kile kilichoamuriwa na mahakama.

Kwa tafsiri ya haraka inamaanisha amekubaliwa kuripoti kazini na kuanza kazi, hivyo amerudi kwenye majukumu yake.

Unadhani suala hili limekwisha? Utakuwa unajidanganya. Kwa vyovyote iwavyo upande wa Rasi wa TFF Karia utakuwa unaangalia pa kutokea na kuweza kumuondoa Karia kwenye majuku yake hayo.

Sidhani na sifikirii kama kunaweza kuwapo kwa mwafaka wa pande hizo mbili. Jambo hili limekuwa likitawala sana katika soka la Afrika.

Sehemu nyingi kumekuwa na migongano kama hii ya Wambura na Karia katika kuongoza soka, viongozi wawili wanakuwa na mitazamo tofaufi. Hili limelifanya soka letu kushindwa kuendelea kwa sababu za visasi na kukomoana.

Wadadisi wa mambo walianza kulitazama jambo hili la Wambura na Karia tangu ulipomalizika uchaguzi uliowaingiza madarakani pale Dodoma.

Wapo walioamini labda wawili hao wangeweza kushikana mikono na kuanza safari upya lakini halikuwezekana, waliishi TFF kwa kuviziana na kupeana muda wa kuweza kushughulikiana.

Kwa dhati kabisa naweza kusema kambi za wawili hao hazikuvunjwa. Bado bifu liliendela tena kwa kushinikizwa na baadhi ya watu wa nje yao.

Hiki ndicho kinachotarajiwa kuendelea hadi sasa baadhi ya hukumu ya Wambura kutoka pale Mahakama Kuu. Lakini je, haya yanafanywa kwa faida ya nani? Wachezaji, klabu, TFF, au Soka la Tanzania kwa jumla?
Ebu tuendelee kusubiri filamu ya upande wa pili. Rais Karia na TFF yake watafanya nini baada ya kupokea nyaraka za Wambura kutoka mahakamani?

ADVERTISEMENT