In Summary
  • Simba wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Mtibwa Sugar ikiwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni michuano mikubwa kwa klabu ambazo zinabeba bendera ya Tanzania kimataifa.

SIMBA na Mtibwa Sugar zitacheza mechi zao kimataifa siku ambayo itakuwa ni mwisho wa usajili wa dirisha dogo, Desemba 15. Timu hizo zinaiwakilisha nchi kimataifa ikiwa ni mechi zake za raundi ya kwanza kwenye michuano husika.

Simba wanashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika wakati Mtibwa Sugar ikiwa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika. Ni michuano mikubwa kwa klabu ambazo zinabeba bendera ya Tanzania kimataifa.

Simba imetinga hatua hiyo baada ya kuwatoa Mbabane Swallows ya eSwatini tena kwa rundo la mabao, sambamba na Mtibwa Sugar ambao pia wamewatoa Washelisheli kwa idadi kubwa ya mabao. Ulikuwa ni ushindi mnono utakaowathibitisha safari yao ijayo.

Simba na Mtibwa Sugar wote wanakwenda kucheza ugenini, ambapo Simba atakuwa mjini Kitwe, Zambia kuwavaa Nkana Red Devils moja ya timu yenye nyota wakali kama straika Walter Bwalya, ambaye aliwahi kuhitajika na Simba lakini walishindwa kutokana na dau lake kuwa kubwa.

Mtibwa Sugar wao watakuwa kwenye Jiji la Kampala, Uganda kuvaana na KCCA nayo kisoka ni timu bora katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kwa sasa.

Lakini, kama kweli timu hizo zinahitaji kufika hatua ya makundi ama mbele zaidi ni kuhakikisha wanakwenda kupambana na kushinda ama kupata sare ya mabao. Yaani wajiandae kwani hii ni vita ya ugenini, ambapo mpinzani ana kila silaha ya kuhakikisha anakujeruhi.

Lakini kuwa ugenini kusiwafanye kuingiwa na hofu, kunyongea na kucheza chini ya kiwango ambapo kwa jinsi zinavyocheza ligi ya hapa basi ndivyo ambavyo inapaswa kuchezwa ugenini na kuongeza mbinu zaidi.

Ushindi unapatikana popote pale kikubwa ni kujiandaa, kujiamini na kuondoa hofu, mambo hayo ni wazi kabisa yanapatikana kwa Simba na Mtibwa Sugar hasa benchi la ufundi jinsi litakavyousoma mchezo na wachezaji kujitambua na kuweka nia ya kusonga mbele zaidi.

Watanzania wote hasa wapenda michezo wote watakuwa wanaelekeza dua zao wikiendi hii kwa timu hizo mbili, lakini dua hizo zitakuwa na maumivu makali kama tu Simba na Mtibwa zitapoteza mechi hizo za ugenini.

Japo inadaiwa ugenini ni ngumu kupata matokeo mazuri, lakini ni vyema kujikinga kwa matokeo mazuri ili mechi ya marudiano itakayochezwa nyumbani iwe rahisi kwenu.

Furaha pekee kwa wanamichezo nchini ni kuona timu hizo mbili kuachana na timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ ambayo imebakiwa na kete moja tu ili ifuzu Afcon dhidi ya Uganda hapo mwakani zinafika mbali na kurejesha matumaini makubwa katika soka.

Watanzania wanawaombea ila na nyie msisahau kujiombea na kupambana kwa juhudi kuhakikisha mnaibuka na ushindi mnono katika michezo hiyo.

Uzembe utakaofanyika katika michezo ya awali mtambue utakuwa mlima mkubwa katika michezo ya marudiano, hivyo ni vyema kujenga mazingira ya kumaliza kazi mapema mkiwa katika michezo ya mwanzo tena ugenini jambo ambalo litasaidia kuwapa moyo watanzania.

ADVERTISEMENT