In Summary

Naibu Kocha wa Bandari FC, Nassoro Mwakoba alisema walistahili kushinda pambano hilo lakini walinyimwa mkwaju wa penalti dakika za mwanzo za mechi hiyo iliyochezwa Mbaraki Sports Club.

MOMBASA. BANDARI FC ilitosheka na matokeo ya sare ya kutofungana na Mathare United FC Jumamosi wiki iliyopita kutokana na sababu ya timu hizo kucheza mchezo wa kufanana ambazo ulizifanya mara nyingi kumalizana kwa sare kwenye mechi zao za Ligi Kuu.

Hata hivyo, Naibu Kocha wa Bandari FC, Nassoro Mwakoba alisema walistahili kushinda pambano hilo lakini walinyimwa mkwaju wa penalti dakika za mwanzo za mechi hiyo iliyochezwa Mbaraki Sports Club.

“Tulistahili kupewa penalti wakati mchezaji wetu alipoangushwa ndani ya eneo hatari la Mathare, lakini hatukupewa. Hata hivyo, hiyo ndiyo hali ya kimchezo tunakubaliana na matokeo ya mchezo huo ya kugawanya pointi moja na wapinzani wetu,” alisema Mwakoba.

Alisema matokeo ya mchezo huo yametokana na timu hizo kuzoeana na mara kadhaa zimekuwa zinatoka uwanjani zikiwa zimetoshana nguvu. “Hakuna ajabu matokeo ya sare ya kutofungana kwani ni uhakika mchezo wa timu zetu mbili hizi huwa ni sawa,” alisema.

Alisema wanashukuru hakuna mchezaji yeyote aliyepata majeraha baada ya mchezo huo na wakati huu wanajitayarisha kwa ziara ya kwenda Nakuru kupambana na Ulinzi Stars FC kwenye Uwanja wa Afraha mwishoni mwa wiki hii.

“Tunashukuru hakuna mchezaji aliyeumia na wanajitayarisha kwa safari ya Nakuru ambayo tunataka tupate ushindi tubakie kileleni mwa ligi,” alisema Mwakoba ambaye aliendelea kuwashukuru mashabiki kwa jinsi wanavyoishangilia timu yao.

Aliwataka mashabiki hao waendelee kuishangilia timu ikiwa nyumbani na ugenini kwa sababu anaamini wachezaji wanacheza vizuri zaidi wakitambua mashabiki wao wako nyuma yao na wanahitaji ushindi.

 

ADVERTISEMENT