In Summary
  • Ingawa kiongozi wa juu ndiye anayeweza kuwa msemaji mkuu, lakini hadi asimame azungumze na jamii inayomzunguka basi ni lazima kuwepo na jambo kubwa la kulizungumzia na sio hata yale mambo ya kawaida tu.

TAASISI mbalimbali nchini na ulimwenguni zina mifumo yake lakini kati ya mifumo hiyo ni lazima kiwepo kitengo cha habari kwa maana, ni wapi taarifa za taasisi zitapatikana na kwa wakati gani.

Ingawa kiongozi wa juu ndiye anayeweza kuwa msemaji mkuu, lakini hadi asimame azungumze na jamii inayomzunguka basi ni lazima kuwepo na jambo kubwa la kulizungumzia na sio hata yale mambo ya kawaida tu.

Katika soka imezoeleka kuwepo na Kamati tofauti kama mashindano, ufundi, usajili, kitengo cha habari na nyingine nyingi tu kulingana na jinsi mfumo wao wa uendeshaji ulivyo. Hivyo hivyo kwenye vyama vingine ambavyo si vyama vya mchezo wa soka, vilivyo vingi vina muundo huo na ndiyo maana hata ukitaka habari basi utazipata kwenye kamati husika kwani ndiyo inayosimamia jambo linalofanywa kwa wakati huo.

Kuwepo mgawanyo wa majukumu kwa kuunda kamati hizo, ni kutaka kila kamati ijihusishe na kushughulikia jambo lake kiufanisi. Hata hivyo, imekuwa tofauti kwa mchezo wa mpira wa kikapu. Ni wazi katiba yao ina mapungufu kidogo.

Mapungufu ya Kikatiba yanaonekana kuwepo kwenye Shirikisho la Mpira wa Kikapu nchini (TBF) ambalo lina kamati nyingi lakini kamati hizo ni kama zipo majina tu, maana hazina mamlaka za kutoa taarifa kwa vyombo vya habari. Mpira wa kikapu unapigiwa kelele kuukuza au kuurudisha kama ilivyokuwa miaka mitano nyuma. Mdau wa mchezo huo alikuwa akisikia kuna mechi, lazima asisimke tofauti na sasa hata wautangaze hakuna tena msisimko. Umepoteza uelekeo kabisa.

Katiba ya TBF inaeleza msemaji wa kila kitu ni Rais wa shirikisho hilo, Phares Magesa, hivyo hata vyombo vya habari vikihitaji kufahamu jambo fulani ambalo ni la kawaida tu, ni lazima awasiliane na Rais huyo.

Ni wazi rais ana majukumu mengi ikiuwamo yale ya kawaida tu anayafanya mwenyewe huku kikapu kikihitaji maendeleo makubwa zaidi.

Katiba haipingiki kwa sababu ilipitishwa na wanachama wao, lakini kibusara tu rais anapaswa kusimama na kuzungumza jambo ambalo anaamini ni zito kwa wadau ama ufafanuzi wake ni mgumu sana kutolewa na mtu mwingine.

Rais anapaswa kugawa madaraka na watakaogawiwa madaraka wasimame kuyafanyia kazi, ila rais anahangaika kuitisha mkutano na vyombo vya habari, kutoa matokeo ya michezo, mambo ambayo yangefanywa na watu wengine. Ni kweli inawezekana rais anapenda kuona kila jambo analisimamia mwenyewe, lakini kazi ya kamati husika ni ipi kama hata mambo ya kawaida anataka kuyatolea ufafanuzi yeye mwenyewe? Hayo ni mapungufu ya kikatiba, majukumu kwake yamekuwa mengi sana na ni wakati wa yeye sasa kutambua hilo.

Mikutano na waandishi wa habari ampe mtu ahangaike nayo kuiitisha, kuzungumzia mashindano awape wenye vitengo vyao kama kamati ya mashindano ama ufundi, yeye abaki kusimamia na kutoa maelekezo kwa watendaji wake na pale inapobidi ndipo asimame kama rais kuzungumza.

Ifike wakati basi, viongozi wa michezo mkubaliane na ukweli kama zinapoundwa kamati basi ziachwe huru kufanyakazi zake hasa inapofika muda wa kushirikiana na vyombo vya habari.

Ni hatari kwa sababu kutakuwepo na udanganyifu wa habari, vitu vya ufundi, mashindano na wanawake ama waamuzi.

Siamini kama Rais anaweza kumudu kuyafafanua mambo yote na kwa wakati, hata kama yeye anadai muda huo anao.

Inaaminika ufanisi wa kazi ambao hauna makandokando unatokana na kila idara kwenye taasisi kufanya majukumu yake ipasavyo, na kila idara ina namna ya kuhamasisha nini cha kufanya ili mambo yaende.

Leo hii mashindano ya Kombe la Taifa yanaendelea huko Simiyu na yanashirikisha timu za wanaume na wanawake kutoka mikoa mbalimbali lakini ni timu moja pekee ya wanawake kutoka Mkoa wa Dar es Salaam ndiyo ipo Simiyu. Timu hiyo sasa inashiriki vipi mashindano bila kuwepo wapinzani, je viongozi wa vyama vya mikoa wanafanya nini kwenye ligi zao za mikoa?

Je huendesha ligi za wanaume pekee, Kamati zao za wanawake kuanzia mikoani hadi ngazi ya TFB wanafanya kazi gani kuhamasisha mchezo huo kwa wanawake.

Ni wazi kama viongozi hao wameingia madarakani kwa kubebwa na huenda hawaelewi vizuri juu ya majukumu yao, ndiyo maana majukumu mengi hufanywa na rais kwa sababu ndiye anayeelewa cha kufanya.

Kutokana na kauli ya rais, hata ukitaka ufafanuzi wa jambo kutoka kamati ya wanawake basi yeye ndiye anawajibika kujibu maswali yake, hii Katiba ya TBF inashangaza.

Rais ni mtu mkubwa sana kwa nafasi yako, gawa majukumu, jipunguzie hata majukumu ya kuitisha mikutano na vyombo vya habari, hata kama kwenye katiba haipo, mchague tu mtu kutoka kwenye kamati zako akusaidie mengine, hilo lisiwe jukumu lako ni jukumu dogo sana.

Ikishindikana basi majukumu mengine yafanywe na makamu wa rais au katibu mkuu ambao naamini wapo na wana uwezo wa kufanya kazi hizo. Kila la kheri kikapu Tanzania.

ADVERTISEMENT