In Summary

Uganda tayari imekata tiketi ya kucheza fainali hizo baada ya kukusanya pointi 13 huku Taifa Stars ikiwa na pointi tano sawa na Lesotho ambayo ilishinda mechi yake dhidi ya Stars kwa bao 1-0 Jumapili iliyopita.

TAIFA Stars imebakiza nafasi moja tu ya kucheza na Uganda katika mechi yao ya mwisho ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwakani.

Uganda tayari imekata tiketi ya kucheza fainali hizo baada ya kukusanya pointi 13 huku Taifa Stars ikiwa na pointi tano sawa na Lesotho ambayo ilishinda mechi yake dhidi ya Stars kwa bao 1-0 Jumapili iliyopita.

Mechi yake ya mwisho Lesotho itacheza na Cape Verde inayoshika mkia kwenye Kundi L lakini matokeo ya mwisho yanaweza kuipa nafasi timu moja kati ya hizo tatu.

Stars sasa inaomba Cape Verde iifunge Lesotho huku yenyewe iifunge Uganda katika mchezo utakaochezwa nyumbani. Ushindi wa Lesotho katika mchezo huo ni majanga kwa Stars ambayo ilifanya makosa makubwa kuruhusu kufungwa katika mchezo wa ugenini.

Wakati Stars ikisubiri mechi yake ya mwisho, wadogo zao wa timu ya vijana chini ya miaka 23 wametolewa na Burundi kwenye michuano ya kuwania kufuzu fainali za vijana kwa umri huo zitakazofanyika Novemba mwakani.

U-23 katika mchezo uliofanyika Burundi walifungwa mabao 2-0 hivyo ushindi wao wa 3-1 juzi Jumanne umewaondoa kwa kuwa Burundi imepata bao la ugenini.

Tukiachana na mambo ya Stars kuna wawakilishi wengine wa nchi kwenye michuano ya kimataifa ambao ni Simba na Mtibwa Sugar.

Hawa ni wawakilishi wa nchi na tegemezi kama ilivyokuwa kwa kwa Timu ya Taifa Stars. Simba inaiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa wa Afrika dhidi ya Mbabane Swallows baada ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu uliopita wakati Mtibwa Sugar itacheza na Timu ya Northern Dyname ya Shelisheli, mechi zote hizo zitachezwa wiki ijayo.

Simba ambayo kwa muda mrefu ilikuwa nje ya anga la kimataifa, itaanzia nyumbani Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam wakati Mtibwa Sugar itacheza mechi yake ya Kombe la Shirikisho ugenini kwenye Visiwa vya Shelisheli. Mechi zote ni ngumu na muhimu kwa wawakilishi hao.

Simba na Mtibwa Sugar zote zipo kwenye ligi na tayari zimepeleka majina ya wachezaji wao watakaocheza michuano hiyo kwa Shirikisho la Soka la Afrika (Caf). Vikosi ambavyo wanaamini vitafanya vizuri.

Tahadhari pekee zinazotakiwa kuzichukua kwa timu hizo ni kutojiamini kupita kiasi kama inavyokuwa kwenye mechi nyingine wanapoteza kwa kuwadharau wapinzani wao, bali wanachotakiwa kufanya sasa ni kuwachunguza wapinzani wao juu ya vikosi vyao.

Simba na Mtibwa wanapaswa kutambua kuwa nao wameshikilia mioyo ya Watanzania wengi kwenye michuano hiyo. Sidhani kama kuna mtu ambaye yupo tayari kukaa roho juu kwa sasa wakati inaaminika timu zina vikosi imara.

Makocha wa timu hizo hawajishughulishi na usajili katika dirisha dogo kwani hata wakiwasajili si wachezaji wa kucheza michuano hiyo bali wataandaliwa kwa ajili ya baadaye watakapopewa nafasi ya kuongeza wachezaji ila si kwa mechi hizi za karibuni.

Hivyo, Simba na Mtibwa zinatazamiwa kuwatumia wachezaji wanaocheza ligi hapa nchini ambao ni asilimia kubwa ya walewale wanaokuwemo kwenye kikosi cha Stars.

Makosa ya Stars kwenye mechi na Lesotho wengi wameyaona, hayategemewi kurudiwa tena na wawakilishi wa nchi kufanya makosa kama hayo.

Iwe kwa makocha kupanga vikosi kwa kujiamini kupita hata kama wanaopangwa hawana uwezo wa kuleta matokeo mazuri ama wana uwezo lakini kuchezeshwa nafasi ambazo hawaziwezi.

Kocha wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems ana misimamo na mfumo wake ambao ameonyesha kwenye ligi, basi asijekurubuniwa ama kuingiwa na hofu hadi ikafikia hatua kukubali kusaidiwa majukumu yake na watu wasiokuwa na utaalamu.

Kauli hivyo vivyo hivyo itumike kwa Kocha wa Mtibwa Sugar, Zubery Katwila.

Kwanza makocha hawa wanatakiwa kufamu kuwa iwapo timu hizi zikifanya vibaya, lawama zote zitaenda kwao na wala sio kwa watu watakaowapa ushauri wa jinsi ya kuwatumia wachezaji.

Makocha hawa wanatakiwa kujiamini na kile wanachokifanya. Wanatakiwa kuachana na dhana inayojengeka kuwa timu za Shelisheli na Eswatini (Swaziland) hazina ubora wa kutosha katika mchezo wa soka.

Binafsi nawaomba makocha hao kuacha kuamini kuwa wamepangaiwa timu vibonde kama walivyoanza kuamionishwa. Umakini unatakiwa katika upangaji vikosi kulingana na mechi bila ya kuweka dharau.

Dhana ya Shelisheli na Uswatini ni vibonde mara nyingi imekuwa ikituponza na kujikuta tumeshaangukia pua. Tuache dhana za zamani ambapo nchi hizi zilikuwa bado hazijapiga hatua kubwa katika soka. Enzi zile ambapo timu zetu zilikuwa zinaweza kuzifunga timu hizo mabao ya kutosha.

Unakumbuka Pamba ya Mwanza iliwahi kuifunga timu ya Shelisheli mabao 17-2? Basi enzi hizo zimeshapita na nchi hizo sasa zimeamka kisoka na siye bado tumebaki palepale.

Mtibwa Sugar itaanzia ugenini ambako ni kugumu ukilinganisha na Simba itakayokuwa nyumbani ingawa nayo inapaswa kuutumia vyema uwanja wa nyumbani kwa kupata matokeo mazuri ili kurahisisha mechi ya ugenini.

Simba imewahi kufika hatua ya makundi mwaka 2003 ambapo sasa hivi inatarajiwa kufika mbali zaidi ya hapo kutokana na ubora wa kikosi chake huku Mtibwa nayo ikiwa na matumaini hayo ya kufika mbali.

Watanzania sasa wanatakiwa kupoza mioyo yao iliyojeruhiwa na Stars kwa klabu hizi mbili kuanzia wiki ijayao ambazo zitaanza rasmi mbio hizo.

Vinginevyo matokeo yakiwa tofauti, basi majeraha kwenye mioyo yao itakuwa maradudu. Sasa ni wakati wa kupumzisha akili za Taifa Stars huku Simba na Mtibwa ikiwa zamu yao kutupa faraja.

ADVERTISEMENT