In Summary
  • Pedja anafahamu jinsi klabu inavyofanya mambo yake. Kwa kile anachokisema Zidane kwenye vyombo vya habari kwa siku za karibuni, kinatafsiri kile kitakachokwenda kutokea katika majira yajayo ya kiangazi.

KUNA mtu anaitwa Pedja Mijatovic. Hivi karibuni kuna kitu amekisema, kuhusu Zinedine Zidane, Real Madrid na Paul Pogba.

Kama alichokisema ni kweli, basi hakika kitakuwa kibao cha usoni kwa Real Madrid. Pedja anaifahamu Real Madrid. Amekuwa kwenye klabu hiyo kwa miaka sita. Mitatu akiwa mchezaji, mitatu mingine akiwa mkurugenzi wa michezo, akifahamu anayeingia na kutoka.

Pedja anafahamu jinsi klabu inavyofanya mambo yake. Kwa kile anachokisema Zidane kwenye vyombo vya habari kwa siku za karibuni, kinatafsiri kile kitakachokwenda kutokea katika majira yajayo ya kiangazi.

Pedja anasema Zidane anapomzungumzia mchezaji, basi ujue anampenda sana. Na Real Madrid ilivyo, mchezaji anapopendwa na kocha, basi anasajiliwa kwa namna yoyote ile.

Kitu kizuri ni kwamba mabosi wa Los Blancos wanamfahamu vizuri Zidane na kazi yake aliyoifanya kwenye timu hiyo katika kipindi chake cha kwanza cha ukocha klabuni hapo.

Siku za karibuni, Zidane amemtaja Eden Hazard na amesema kitu pia kuhusu Paul Pogba.

Man United ijiandae tu kisaikolojia. Wakijumlisha kile alichokizungumza Pogba kwenye mechi za kimataifa, kinaonyesha wazi kile kinachokwenda kutokea mwishoni mwa msimu, kwa kweli wajiandae tu, wasije wakashitukizwa halafu wakapata maumivu.

Kitu pekee kitakachokuja kukwamishwa ni ada yake ya uhamisho. Kiwango kipi kitafaa. Euro 100 milioni au Euro 150 milioni. Kuna sauti inasema kwamba inawezekana kabisa ikawa ni Euro 180 milioni.

Pogba Pauni 180 milioni. Suala litabaki kwa Florentino Perez atakubali kutoa pesa hiyo?

Miaka mitatu iliyopita alipuuza kutoa Euro 105 milioni kunasa huduma yake alipokuwa Juventus. Kwa wakati ule isingekuwa rahisi kwa Perez kutoa pesa ndefu hivyo. Kwenye kikosi chake kulikuwa na mastaa wengi wenye viwango bora.

Kulikuwa na wengi, akiwamo Toni Kroos pia. Lakini, sasa Kroos anaonekana amechoka. Gareth Bale ameshindwa kufanya kweli na kuwalazimisha Los Blancos kufanya usajili mwingine wa mastaa wenye kiwango cha dunia.

Kwa kauli ya Pedja hakuna ubishi, Real Madrid itaingia sokoni kumsaka Pogba mwishoni mwa msimu huu hasa ikizingatiwa kocha wake anamtaka mchezaji huyo ambaye amebeba ubingwa wa dunia akiwa na kikosi cha Ufaransa katika michuano iliyomalizika katikati ya mwaka jana.

Pogba ni mchezaji muhimu Manchester United. Lakini, wababe hao wa Old Trafford wanaweza kufuta machungu ya kumpoteza Pogba kama watahitaji wabadilishwe na Kroos na Bale.

Wachezaji hao wawili wanajenga thamani ya Euro 150 milioni.

Los Blancos hawaonekani kuwa na biashara tena na Kroos. Hawaonekani kumhitaji tena Bale na ndio maana wanamtaka Hazard pia kwa ajili ya kuziba mapengo hayo.

Hivyo kumpata Pogba kwa kuwatumia wachezaji hao itakuwa faida kubwa kwao kuliko kutoa pesa kisha ikabaki na wachezaji hao kwenye kikosi kuwaongezea tu bili ya mishahara.

Lakini, Man United nayo itakuwa imepata faida kubwa kwa kuwapata Kroos na Bale kwa pamoja. Hapo kila mtu atakuwa amepata faida kwa upande wake.

Januari mwaka jana Manchester United ilifanya dili la aina hiyo na Arsenal. Ilipobadilishana Henrikh Mkhitaryan na Alexis Sanchez.

Matokeo ya wachezaji hao kila upande umekuwa na maumivu hawakuweza kufikia kiwango ambacho kilitarajiwa na kuzua mshangao kwa mashabiki.

Si Sanchez wala Mkhitaryan aliyefanya vizuri kwenye timu yake mpya. Lakini, hili dili la Pogba kwa wachezaji Kroos na Bale bila ya shaka litakuwa na faida kubwa huko katika kambi ya Old Trafford.

Faida yake ipo hata kwenye mishahara. Pogba anataka alipwe Pauni 500,000 kwa wiki, mshahara wake yeye tu.

Lakini, Manchester United inaweza kutumia mshahara huo kuwalipa Kroos na Bale kama wakitua katika klabu hiyo. Inaweza kumlipa Kroos Pauni 200,000 na Bale Pauni 300,000.

Hii ndiyo njia pekee ambayo Man United inaweza kufaidika kwa kumpoteza kiungo wake Pogba.

Hapo timu itakuwa haijapata pengo, imepoteza mchezaji wa kiwango cha dunia, lakini itakuwa imepata wengine wawili wenye viwango vya dunia.

Kroos na Bale wanaonekana kuchoka Madrid, lakini huenda kabisa wasiwe wachovu wakitua katika klabu ya Manchester United.

Huko katika kambi ya Real Madrid hakuna tena kitu kipya cha kupigania, maisha mapya yatakuwa na umuhimu kwao na ndio maana kama Perez atakubali dili la kubadilishana basi Manchester United wanapaswa kukimbia haraka sana kukamilisha jambo hilo. Litakuwa na faida kubwa kwao kwani wachezaji hao watataka kuonyesha vitu vipya.

ADVERTISEMENT