In Summary
  • Hata wachambuzi na wachezaji wa zamani wa Manchester United walitoa maoni yao kuhusu nani apewe timu hiyo na kura nyingi zikimtaja Pochettino.

HIVI ndivyo maisha yanavyokwenda kasi. Desemba mwaka jana, wakati Jose Mourinho anafutwa kazi huko Old Trafford na kitu chake kupewa Ole Gunnar Solskjaer kwa muda, kelele nyingi zilikuwa zikimtaka Mauricio Pochettino kwamba ndiye aliyekuwa akienda kupewa kibarua hicho mwisho wa msimu huu.

Zilitajwa hadi gharama ambazo Manchester United inapaswa kulipia kuvunja mkataba wa Muargentina huyo huko Tottenham Hotspur.

Hata wachambuzi na wachezaji wa zamani wa Manchester United walitoa maoni yao kuhusu nani apewe timu hiyo na kura nyingi zikimtaja Pochettino.

Lakini, ndani ya miezi miwili na nusu tu, Pochettino ametoka kuwa chaguo la wengi hadi kuonekana kuwa wa kawaida tu.

Solskjaer amemwonyesha na yeye yupo siriazi kiasi gani katika kukitaka kibarua hicho cha kudumu klabuni hapo. Matokeo ya hivi karibuni ya Spurs yamemwondoa Pochettino kwenye nafasi hiyo kubwa ya kuwa kocha mpya wa Man United.

Huko Old Trafford mabosi wengine wameonekana kuangukia kwenye mapenzi ya Solskjaer. Kinachotia moyo kuhusu Ole ni kwamba yupo na timu ileile iliyokuwa si kitu chini ya Mourinho, lakini imekuwa ikipata matokeo bora uwanjani.

Man United imekuwa ikicheza mechi zake bila ya kusikia kauli za malalamiko kutoka kwenye benchi la ufundi.

Ole anafanya kazi na wachezaji waliopo. Kipindi cha Mourinho, kila siku kocha huyo alikuwa anatoa malalamiko tu. Ugomvi na wachezaji kilikuwa kitu kikubwa kwake. Zama za Mourinho na hawa majeruhi waliopo kwenye kikosi hicho cha Man United, basi kingekuwa kisingizio kikubwa cha timu hiyo kufanya vibaya.

Lakini, Manchester United ina majeruhi kibao, wachezaji 10 wa kikosi cha kwanza, lakini husikii kelele za malalamiko kutoka kwa Kocha Ole. Anapiga mzigo. Amewakabili Liverpool na majeruhi yake na ameshinda mechi zilizofuatia, tena kibabe.

Hivi ndivyo kocha anavyopaswa kufanya mambo yake. Kuhusu Pochettino ameonekana kuugua ugonjwa uleule wa miaka yote. Kila wakati timu inapokuwa kwenye nafasi kubwa ya kuonyesha upinzani kwenye mbio za ubingwa, anashindwa kuwaandaa vyema wachezaji wake kufikia mafanikio hayo.

Kwa misimu mitatu mfululizo iliyopita, Spurs imekuwa na tatizo lilelile.

Hivi karibuni, kikosi hicho cha Pochettino kilikuwa na nafasi ya kuzivuruga Liverpool na Manchester City kwenye mbio za ubingwa. Timu yake imepoteza mechi mbili mfululizo na kila kitu kimeishia hapo.

Hivi sasa amemzidi pointi tano tu mtu ambaye alionekana kwenye kiti alichopo hafai ili achukue yeye mikoba. Solskjaer amezidiwa pointi tano tu na Pochettino.

Kitu kizuri ni kwamba Ole amemwambia wazi Pochettino kwamba anakuja kuchukua namba tatu. Hii ina inaonyesha kwamba Ole amemfanya Pochettino sio mpinzani wake kwenye kukinasa kibarua cha kudumu huko Old Trafford.

Kwa rekodi hizo, Manchester United hawawezi kuwa wajeuri na kumpa kazi Pochettino na kumtema Solskjaer. Hawataeleweka na mashabiki kabisa. Kitu ambacho kilikosekana siku nyingi kwenye kikosi cha Manchester United, Ole amekirudisha.

Man United swagi. Kuingia uwanjani kwa dhamira ya kushinda mechi na si kutoka sare. Manchester United haiogopi kufungwa, isipokuwa yenyewe inachokifanya ni kujaribu kufunga mara nyingi kuliko mpinzani wake.

Hivi ndivyo Ole alivyoibadili akili ya wachezaji wa Manchester United. Ndio maana kila mchezaji amekuwa na umuhimu na nafasi yake ya kutoa mchango kwenye timu. Hivi ndivyo Solskjaer alivyolinda kibarua chake na kumtupa nje Pochettino.

ADVERTISEMENT