In Summary
  • Emery hakutaka kabisa kumgusa Mesut Ozil kwenye mechi hiyo. Hakuwapo kabisa. Nafasi yake aliwapanga watu wawili, Alex Iwobi na Henrikh Mkhitaryan na kucheza fomesheni ya 3-4-2-1. Miki na Iwobi hawakucheza kama Emery alivyotaka, hivyo akawatoa na kuwaingiza Ramsey na Lacazette wakati wa mapumziko. Kuingia kwa wawili hao, Arsenal ikabadili mfumo na kucheza 3-4-1-2.

ARSENAL 4, Spurs 2. Siyo ishu. Hayo ni matokeo ya kawaida kwa Arsenal mbele ya mahasimu wao hao wa London.

Hata kipindi cha Arsene Wenger, Arsenal imekuwa mbabe wa Spurs mara nyingi. Ishu hapa ni kuona mechi ya msimu huu ya mahasimu hao kuwa ya kimbinu zaidi.

Makocha Unai Emery na Mauricio Pochettino walitumia ufundi zaidi kuikabili mechi hiyo. Ukweli wawili hao ni marafiki na wanafahamiana vizuri, kwa sababu walianza kuchuana tangu kwenye La Liga. Kwenye Ligi Kuu England ilikuwa mara yao ya kwanza, lakini linalowafurahisha mashabiki wa mpira waliotazama mechi hiyo makocha hao walivyobadili mifumo ya uchezaji kusaka matokeo huku mchezo ukiendelea. Hicho ndicho kitu kilichotokea Emirates. Matokeo yalikuwa ni kitu cha ziada tu.

Emery hakutaka kabisa kumgusa Mesut Ozil kwenye mechi hiyo. Hakuwapo kabisa. Nafasi yake aliwapanga watu wawili, Alex Iwobi na Henrikh Mkhitaryan na kucheza fomesheni ya 3-4-2-1. Miki na Iwobi hawakucheza kama Emery alivyotaka, hivyo akawatoa na kuwaingiza Ramsey na Lacazette wakati wa mapumziko. Kuingia kwa wawili hao, Arsenal ikabadili mfumo na kucheza 3-4-1-2.

Hayo yalikuwa mabadiliko ya kiufundi ambayo yalileta matatizo kwa Spurs. Mabeki wa Pochettino walikuwa na kibarua cha kumkabili mshambuliaji mwingine aliyeongezeka. Kuona hivyo, Spurs iliyoitumia 4-3-1-2 ikacheza 4-2-3-1.

Lakini, jambo kubwa ni namba Emery alivyoweza kulisoma tatizo kwa haraka na kuwatoa Miki na Iwobi. Mwanzoni, Arsenal ikicheza 3-4-2-1 waliwapa shida Spurs na fomesheni yao ya 4-3-1-2 hasa kwa upande wa pembeni na hapo, Pochettino alibadilika haraka kutumia 4-2-3-1. Baadaye, Arsenal wakaanza kutumia 3-4-1-2 baada ya kuingia kina Lacazette na Pochettino akarudi kwenye ile fomesheni ya 3-4-1-2. Arsenal ikapata pigo. Shkodran Mustafi aliumia na kutolewa, lakini hilo halijakuwa shida kwa Emery, kwani alimwiingiza kiungo Guendouzi na kubadilisha mfumo, Arsenal wakaanza kucheza 4-3-1-2. Fomesheni hiyo iliwazima kabisa Spurs na mshambuliaji mmoja wa nyongeza wa Arsenal alionekana kuwapa shida mabeki wa Spurs.

Wakachapwa bao tatu za maana, ubao ukabadilika kutoka 2-1 na kuwa 4-2, Emery akishinda dabi yake ya kwanza dhidi ya Spurs kwenye Ligi Kuu England. Matokeo hayo na kubadilika huko kwa Emery kumemfanya kuanza kuwaaminisha mashabiki sasa anaanza kutengeneza mfumo wake kwenye kikosi hicho baada ya utawala wa muda mrefu wa Arsene Wenger.

Mashabiki wanaamini hii si Arsenal ile, hii ni mpya. Na hizi si zama zile ni zama za Emery. Mtihani mwingine mbele yao upo wiki hii. Kesho Jumatano itacheza na Man United ya Jose Mourinho. Inafahamika, Arsenal hawaipendi Man United na hawampendi Mourinho. Hivyo, hakuna kitu kitakachowapa furaha zaidi kama watashinda mchezo huo utakaofanyika Old Trafford.

ADVERTISEMENT