In Summary
  • Kwa maoni yangu namuunga mkono Oliech kwani, hakuwahi kusema anastaafu soka, bali mi naona alienda mapumziko na sasa amemaliza mapumziko hayo na kuamua kurejea kwani soka ni kazi kama kazi nyingine.

HIVI karibuni, mchezaji Denis Oliech aliamua kutafuta viatu vyake alivyokuwa ameviweka katika paa la nyumba na kuamua kurejea uwanjani.

Jambo hilo limepokewa kwa hisia tofauti miongoni mwa mashabiki na wadau wa soka, kwani wapo waliokataa arejee kama mchezaji wakimtaka arejee kama kocha.

Hata hivyo, wengine wengi walikubali uamuzi wake wa kurejea kama mchezaji.

Kwa maoni yangu namuunga mkono Oliech kwani, hakuwahi kusema anastaafu soka, bali mi naona alienda mapumziko na sasa amemaliza mapumziko hayo na kuamua kurejea kwani soka ni kazi kama kazi nyingine.

Kiumri, Oliech hajafika umri wa kustaafu na kwa sasa anahitaji tu mazoezi mafupi na muda mfupi tu atarejea kwenye kiwango chake kwani ni mmoja kati ya washambuliaji bora zaidi wa Kenya.

Tayari kashatua Gor Mahia na pale anachokihitaji ni viungo kumwelewa anataka nini. Kama utakumbuka, enzi zake alikuwa anazungukwa na viungo kama Titus Mulama na Robbert Mambo ambao walikuwa wakimwelewa sana.

Oliech ana kasi sana na hodari wa kufunga. Kwangu naona Gor imepata mchezaji ambaye iwapo watamtumia vizuri watafurahia.

Natumai wachezaji kama Kahata na zile pasi zake za uhakika, ataweza kumfanya Oliech arudi katika hali yake ya kawaida.

Kenya kuna uhaba wa washambuliaji na kama atapata ushirikiano kamili kutoka kwa washambuliaji wengine, basi wengi watajifunza mengi kutoka kwake.

Tanzania, kurudi kwa Mrisho Ngassa kwenye klabu yake ya Yanga, wengi hawakutaka wakiamini uwezo wake umekwisha.

Hata hivyo, kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu alirejea kwa kishindo na sasa anafanya mambo makubwa. Uzoefu alionao Ngassa kwenye Ligi Kuu Tanzania, wengi hawana hivyo kuifanya Yanga kutamba Ligi Kuu kutokana na kazi yake. Yote hayo ni uzoefu tu, na mfano mwingine ni kiungo, Athumani Iddy Chuji, pia bado anakipiga tena vizuri sana.

Soka ni kujiamini tu, ukiwa na wachezaji wanaokuelewa, viongozi na kocha anayekupa nafasi, huna cha kukuangusha.

Asamoah Gyan na Obi Mikael ni wakongwe katika soka lakini hasdi sasa bado wanacheza kwa viwango bora kabisa. Hii ni kwa sababu wanajiamini. Katika maisha ukijikubali na ujiamini hakuna kitu kitakusimamisha.

Hivyo, kwangu mimi namtakia Denis ‘The Manace’ shughuli safi kwenye Ligi Kuu Kenya na endapo atarudi kwenye kiwango chake, hata kwenye timu ya taifa, Harambee Stars anaweza akaitwa.

Kwa nini nasema anaweza akaitwa Stars, ni kwa sababu kuna uhaba wa washambuliaji, ni wazi kuna mmoja tu anayetegemewa, Michael Olunga. Hivyo, ni lazima awepo mwingine wa kumsaidia.

Ukweli bila kuficha, ndani ya miezi miwili Oliech atakuwa amerudi katika kiwango chake na ili iwe hivyo, ni yeye mwenyewe ajiweke katika mazingira mazuri na kuachana na mambo mengi yatakayomzuia kucheza soka lake.

Hata hivyo, kurejea kwake kutawaamsha washambuliaji wa Kenya ambao kwa kweli wamelala. Kazi kwao kumtumia Oliech kuamka.

Oliech kwa nnavyomwona, ana misimu mitano ya kucheza soka la ushindani na akafanya makubwa.

Kurudi kwake sidhani kama ni kwa sababu ya kimasilahi au kuonekana tu, bali amedhamiria kufanya makubwa kwa Kenya.

Mkataba wa miaka miwili pale Gor ni dhihirisho tosha Oliech anaenda kupiga kazi. Gor wameona kitu kwake na ndio maana wakaamua kumpa mkataba wa pesa nyingi. Kwa nini wasimpe wa mwaka au miezi sita. Wameona kitu.

Tanzania, kiungo Haruna Moshi ‘Baoban’ aliyetamba na Simba na Taifa Stars miaka ya nyuma, ametua Yanga. Kumbuka Yanga ni timu kubwa na inatakiwa isajili nyota wakubwa.

Sasa jiulize kwa nini Boban ambaye umri umesonga sana?

Kumbuka, Yanga sio kwamba hawajaona wachezaji wengine, ila kocha ameona kitu kwa Boban na kuamua kumsajili. Ni mkataba wa miezio sita tu lakini kuna alichokiona kwa Boban kitamsaidia.

Hivyo, Oliech kupewa kandarasi ya miaka miwili ni wazi kocha ameona kitu na atafanya kazi kubwa sana. Yetu ni kumtakia kila la Kheri.

ADVERTISEMENT