In Summary
  • Akizungumza wakati wa tuzo za African Women Film Festival, Lulu alisema Monalisa ameanza kazi za sanaa muda mrefu, lakini amekuja na wazo hilo la kutoa tuzo sasa hivi.

MAISHA ni kupeana shavu na hilo limeonekana kumpa mzuka zaidi staa wa kike, Elizabeth Michael (Lulu), aliyefichua kuwa amekuwa akifuata maelekezo ya Monalisa katika kufanikisha mambo yake kisanii.

Lulu, ambaye ni miongoni mwa wasanii wanaosumbua kwenye mitandao ya kijamii, alisema kuwa Monalisa amekuwa akiwafundisha kuwa na subira kwenye maisha.

Akizungumza wakati wa tuzo za African Women Film Festival, Lulu alisema Monalisa ameanza kazi za sanaa muda mrefu, lakini amekuja na wazo hilo la kutoa tuzo sasa hivi.

“Wasanii huwa tunakuwa na mambo mengi ya kufanya pale tunapopata umaarufu, lakini Monalisa hilo kwake halikuwa sababu, kwani amekaa kimya kwa muda wote mpaka sasa alipoamua kuja na tuzo hizi ambazo naamini huko mbele zitakuwa kubwa,” alisema.

Katika tuzo hizo Lulu pia alionekana kuwa kivutio, baada ya kuongozana na baunsa aliyekuwa anamlinda wakati wote.

Hata hivyo, tofauti na wasanii wengine ambao walikuwa wakisimama kwenye zulia jekundu na kufanya mahojiano na waandishi kwa msanii huyo ilikuwa tofauti, kwani hata muda wa kuondoka hakuna aliyejua kaondoka saa ngapi.

Mbali ya kualikwa kwa ajili ya kutoa tuzo, pia alikuwa kati ya wasanii waliokuwa wakiwania kipengele cha msanii bora wa filamu kipengele ambacho Riyama Ally aliibuka kidedea.

Wengine walioshindanishwa katika kengele hicho ni Neema Ndepanya, lamata Leah na Godliver Gordian.

ADVERTISEMENT